Wednesday, November 14, 2012

MBOWE KUIFUTA TAKUKURU MARA AKIINGIA MADARAKANI.

MBOWE ASEMA CHADEMA IKICHUKUA MADARAKA ITATIMUA WATENDAJI WOTE WA TAKUKURU KWA VILE WAMESHINDWA KUZUIA RUSHWA CCM.


Mwenyekiti wa chadema,Freeman Mbowe akiwa na keki aliyokabidhiwa na wakulima wa ngano Babati,ambao walimuomba awasaidie kutetea kurejeshwa mashamba ya Ngano yaliyokuwa na shirika la chakula la Taifa(NAFCO) ambayo sasa yamebinafsishwa na hayaendelezwi. Kulia ni   diwani wa viti maalum Hanang, Sara Joseph

Mwandishi wetu, Hanang’
MWENYEKITI wa Chadema, Freeman Mbowe amependekeza kuvunjwa kwa Taasisi za Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru), kwani badala ya kupambana nayo inaipalilia.
Akifungua tawi ya Chadema Kata za Katesh linalopakana na ofisi za Takukuru Wilaya ya Hanang, Mkoa wa Manyara juzi, Mbowe alisema taasisi hiyo imeshindwa kazi.


Mbowe alisema Takukuru imeshindwa kudhibiti hata rushwa ya wazi ndani ya CCM kwenye chaguzi ambazo zilifanyika hivi karibuni.
“Hakuna ambaye hakujua rushwa ndani na CCM na jinsi ambavyo imeathiri chama hicho, lakini Takukuru wameshindwa kupambana na rushwa hiyo badala yake wanailea,” alisema Mbowe.


Alisema Rais Jakaya Kikwete ambaye anasimamia Takukuru iliyopo kwenye wizara yake, ameshindwa kuibana ndiyo sababu hata yeye amekuwa akilalamika.
Pia, Mbowe alifungua matawi kata za Endasaki na Ganana, alisema kutokana na Takukuru kushindwa kupambana na rushwa, isipovunjwa chama hicho kikiingia madarakani kitawatimua watendaji wote wa taasisi hiyo ili wafanye kazi nyingine.


Alisema Takukuru imeshindwa hata kusaidia kurejesha mabilioni ya fedha za Watanzania ambayo yamefichwa nchini Uswis.


“Hawa Takukuru walipaswa kuanza kufanya uchunguzi juu ya fedha hizo baada ya kupata taarifa na kusaidia taifa kuzipata, lakini wamekaa kimya,” alisema Mbowe.


Alisema kutokana na ukimya huo, ndiyo sababu Chadema kupitia Naibu Katibu Mkuu wake, Kabwe Zitto waliomba serikali kufanya uchunguzi na kutoa taarifa bungeni juu ya walioficha fedha na utaratibu wa kuzirejesha.


“Bunge lijalo, kama wasipoleta taarifa ya maana juu ya fedha za Uswis tunajua la kufanya, nadhani mmeona jinsi hoja hii ilivyoungwa mkono na watu wengi,”alisema Mbowe.


Awali, Mbowe alizitaka ofisi hizo za Chadema, alizofungua kuwa kimbilio la wanyonge kutoa kero zao na kusaidiwa badala ya kuwa maeneo ya kukaa viongozi pekee.
Chanzo. Gazeti la Mwananchi

No comments:

Post a Comment