Sumaye ameitaka Afrika kutokomeza rushwa
Waziri Mkuu Mstaafu, Frederick Sumaye amezitaka nchi za Afrika ikiwemo Tanzania kupambana na makundi na kuwalipua wala rushwa na wapokeaji kwa kuwachukulia hatua.
Alitoa kauli hiyo jana jijini Dar es Salaam katika maadhimisho ya miaka 20 ya Chuo Kikuu Huria cha Tanzania, (OUT).
Katika mada yake iliyokuwa ikizungumzia kuhusu changamoto za kupunguza umaskini nchini, Sumaye alisema nchi za Afrika zipo nyuma kimaendeleo na kwamba yapo mambo mengi yanayotakiwa kufanyika.
Alitaja baadhi ya mambo hayo kuwa ni nchi kuwa na serikali inayopambana na makundi yote mabaya hasa rushwa.
"Lazima tuipige vita rushwa ili kile kidogo kinachotakiwa kipatikane basi kipatikane kwa ajili ya huduma za wananchi na sio kupotea njia," alisema.
Alitaka nchi zifanye biashara ambazo zitaweza kuzimudu na kutolea mfano Tanzania.
"Tusiuze tu vitu kwa mfano magogo, pamba na madini nje ya nchi, tunatakiwa vitu hivi tuvibadilishe kuwa thamani ndio tuvipeleke nje kwenye soko la biashara, tunaiuzia magogo China halafu yeye anayabadilisha kuwa vitu vya thamani anakuja kutuuzia sisi tena, kwa nini sisi tusifanye vyote hivyo, tuwauzie wao," alisema.
Kuhusu rushwa na utawala bora, Sumaye alisema lazima nchi ifikie mahali iwe na utaratibu wa kuhakikisha jambo hilo halivumiliki kwa sababu limekuwa likiigawa jamii katika kundi la wenye utajiri na maskini.
Mtazamo wake kama Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru) kwa sasa inafanya kazi yake ipasavyo kutokana na kuanzishwa wakati akiwa madarakani, alisema anafikiri inafanya kazi yake.
Kuhusu nini kifanyike, Sumaye alisema nchi inatakiwa kuwa na utawala bora ambao utawezesha rasilimali za nchi zinatumika kwa manufaa ya watu wote.
Pia alisema nchi inatakiwa kuhakikisha inakuwa na utawala wa sheria na kuheshimu haki za binadamu na kuwepo na matumizi sahihi ya mali za taifa ili kila Mtanzania aweze kunufaika nazo.
Naye, Mkuu wa Chuo hicho, Profesa Tolly Mbwette, alisema kuwa, katika maadhimisho hayo miadhara ya majadiliano iliyotolewa imelenga jamii na serikali kwa ujumla.
Alisema lengo lake ni kutoa michango yao kwenye maeneo tofauti ambayo serikali imejiwekea katika kuyafikia maendeleo.
Profesa Joseph Mbwiriza wa OUT akichangia majadiliano hayo, alisema suala la umaskini ni kubwa na watu wengi wapo nje ya mfumo rasmi wa uchumi.
"Wanawake wengi hatuwatambui, kazi wanazozifanya haziingii kwenye takwimu zetu za kiuchumi za taifa, nini kifanyike tutekeleze Mpango wa Kurasimisha Rasilimali na Biashara za Wanyonge Tanzania (Mkurabita) ili kazi zao na za wengine zitambuliwe kisheria, " alisema.
Katika maadhimisho hayo mijadala mbalimbali ilitolewa ukiwemo uliokuwa ukiangalia kupotea kwa maadili kwenye jamii ya Tanzania.
CHANZO: NIPASHE JUMAPILI
No comments:
Post a Comment