Sunday, June 16, 2013

DK. HOSSEAH WA TAKUKURU AFUNGUKA, ASEMA TAKUKURU INATENGWA NA SERIKALI.



Mkurugenzi Mkuu wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru), Dk Edward Hoseah 

Dodoma. Mkurugenzi Mkuu wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru), Dk Edward Hoseah, amefunguka na kueleza sababu za taasisi yake kushindwa kuwakamata walarushwa wakubwa kwa kuwa Serikali imemfunga mikono.
Akitoa majumuisho katika Mkutano Mkuu wa Chama cha Wabunge Wanaopambana na Rushwa nchini (APNAC) jana, Dk Hoseah alisema kuwa Serikali imeitenga Takukuru na kuwafanya waishi kama yatima.
Huku akishangiliwa na idadi kubwa ya wabunge, mkurugenzi huyo alisema kuwa amekuwa akishangazwa na lawama ambazo amekuwa akibebeshwa kila wakati kuwa ameshindwa kumaliza rushwa wakati bila kuziangalia sheria.
“Mnanipa lawama kila wakati, lakini huwezi kuanzisha chombo kama Takukuru halafu ukamfunga mikono mhusika, na mimi mmenifunga mikono nifanyeje jamani? Alihoji na kuongeza:
“Hata katika rasimu ya Katiba bado mmetutenga kama watoto yatima, wenzetu wote mmewaweka tena hata CAG mmesema kuwa mamlaka yake akiteuliwa basi asiingiliwe wala kuhojiwa…mamlaka gani mtu asihojiwe jamani, mimi nikiuliza Takukuru mnasema subirini Serikali ya Tanganyika.”
Gazeti la Guardian la Uingereza la Jumapili ya Desemba 19, 2010, lilitoa taarifa ya siri kuhusu wala rushwa wakubwa kulindwa Tanzania. Gazeti hilo lilichapisha taarifa za mtandao wa WikiLeaks uliokuwa ukimilikiwa na mwandishi wa habari wa Australia, Julian Paul Assange, ukimnukuu Dk Hoseah.
Dk Hoseah alinukuliwa na WikiLeaks akimueleza mwanadiplomasia wa Marekani aitwaye Purnell Delly, Julai 14 jijini Dar es Salaam mwaka 2007 kuhusu uwezo na nia ya Rais Kikwete katika kushughulikia ufisadi.
Alidai Rais Jakaya Kikwete alikuwa anakwamisha kuchunguzwa kwa vigogo wa Serikali wanaotuhumiwa kwa vitendo vya rushwa, na pia anahofia maisha yake kama mkuu wa Takukuru. Hata hivyo, Dk Hoseah kwanza alikiri kukutana na ofisa huyo ofisini kwake Julai 2007, lakini alikanusha kuzungumza kuwa Rais Kikwete alikuwa hataki sheria ichukue mkondo wake katika kuwachunguza vigogo wanaotuhumiwa kwa rushwa.
Atoa ushauri kwa Serikali
Kwa mara ya kwanza jana kiongozi huyo aliitolea uvivu Serikali kuwa imekuwa ikichangia mambo mengi katika rushwa ikiwamo usiri mkubwa katika rasilimali za nchi.
“Lazima Serikali iwe wazi, huwezi kuwaficha wananchi rasilimali zao eti ni siri kwa sababu ya sera mbovu, tunawaambia wananchi watanufaika na mirabaha ya asilimia tatu hiyo siyo sahihi jamani ndiyo maana tunashindwa kutoa majibu kwa wananchi wetu hilo ni tatizo jingine linalosababisha mambo ya rushwa,”alisema na kuongeza: “Siyo kila jambo ambalo serikali inapewa ushauri ni baya.”
Alipinga kitendo cha viongozi kuwa na kigugumizi katika uwajibikaji na akataka itungwe sheria kali ya kutaka kiongozi awajibike mara anapokuwa ametuhumiwa kwa jambo lolote aachie ngazi na kupisha uchunguzi kama ilivyo kwa nchi zingine.
Credits; Gazeti la Mwananchi

ELIMU YA NAMNA YA KUEPUKA RUSHWA KWA SEKTA YA AFYA WILAYANI NACHINGWEA.

 Wadau wa Afya toka maeneo mbalimbali ya Nachingwea walikutana katika Ukumbi wa TRC mjini Nachingwea na moja ya somo walilofundishwa ni Mapambano dhidi ya Rushwa.

Wanafunzi Chuo cha UUguzi Nachingwea wakipata elimu ya Mapambano dhidi ya Rushwa toka kwa Maafisa wa TAKUKURU waliowatembelea hivi karibuni.

ELIMU YA MAPAMBANO DHIDI YA RUSHWA YATOLEWA KWA WANAFUNZI WA SEKONDARI WILAYANI NACHINGWEA.

 

Afisa wa TAKUKURU Bw. Hassan Omari wa Nachingwea akipokea risala toka kwa kiongozi wa Klabu ya Wapinga wa Rushwa shule ya sekondari Marambo wakati wa ziara ya uhamasishaji wa mapambano dhidi ya rushwa hivi karibuni.

Baadhi ya wanafunzi shule ya sekondari Marambo huko Nachingwea wakisikiliza mawaidha toka kwa maafisa wa TAKUKURU(hawapo pichani).

Wednesday, November 14, 2012

MBOWE KUIFUTA TAKUKURU MARA AKIINGIA MADARAKANI.

MBOWE ASEMA CHADEMA IKICHUKUA MADARAKA ITATIMUA WATENDAJI WOTE WA TAKUKURU KWA VILE WAMESHINDWA KUZUIA RUSHWA CCM.


Mwenyekiti wa chadema,Freeman Mbowe akiwa na keki aliyokabidhiwa na wakulima wa ngano Babati,ambao walimuomba awasaidie kutetea kurejeshwa mashamba ya Ngano yaliyokuwa na shirika la chakula la Taifa(NAFCO) ambayo sasa yamebinafsishwa na hayaendelezwi. Kulia ni   diwani wa viti maalum Hanang, Sara Joseph

Mwandishi wetu, Hanang’
MWENYEKITI wa Chadema, Freeman Mbowe amependekeza kuvunjwa kwa Taasisi za Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru), kwani badala ya kupambana nayo inaipalilia.
Akifungua tawi ya Chadema Kata za Katesh linalopakana na ofisi za Takukuru Wilaya ya Hanang, Mkoa wa Manyara juzi, Mbowe alisema taasisi hiyo imeshindwa kazi.


Mbowe alisema Takukuru imeshindwa kudhibiti hata rushwa ya wazi ndani ya CCM kwenye chaguzi ambazo zilifanyika hivi karibuni.
“Hakuna ambaye hakujua rushwa ndani na CCM na jinsi ambavyo imeathiri chama hicho, lakini Takukuru wameshindwa kupambana na rushwa hiyo badala yake wanailea,” alisema Mbowe.


Alisema Rais Jakaya Kikwete ambaye anasimamia Takukuru iliyopo kwenye wizara yake, ameshindwa kuibana ndiyo sababu hata yeye amekuwa akilalamika.
Pia, Mbowe alifungua matawi kata za Endasaki na Ganana, alisema kutokana na Takukuru kushindwa kupambana na rushwa, isipovunjwa chama hicho kikiingia madarakani kitawatimua watendaji wote wa taasisi hiyo ili wafanye kazi nyingine.


Alisema Takukuru imeshindwa hata kusaidia kurejesha mabilioni ya fedha za Watanzania ambayo yamefichwa nchini Uswis.


“Hawa Takukuru walipaswa kuanza kufanya uchunguzi juu ya fedha hizo baada ya kupata taarifa na kusaidia taifa kuzipata, lakini wamekaa kimya,” alisema Mbowe.


Alisema kutokana na ukimya huo, ndiyo sababu Chadema kupitia Naibu Katibu Mkuu wake, Kabwe Zitto waliomba serikali kufanya uchunguzi na kutoa taarifa bungeni juu ya walioficha fedha na utaratibu wa kuzirejesha.


“Bunge lijalo, kama wasipoleta taarifa ya maana juu ya fedha za Uswis tunajua la kufanya, nadhani mmeona jinsi hoja hii ilivyoungwa mkono na watu wengi,”alisema Mbowe.


Awali, Mbowe alizitaka ofisi hizo za Chadema, alizofungua kuwa kimbilio la wanyonge kutoa kero zao na kusaidiwa badala ya kuwa maeneo ya kukaa viongozi pekee.
Chanzo. Gazeti la Mwananchi

Sunday, November 4, 2012

MBUNGE ZUNGU WA ILALA AKAMATWA KWA RUSHWA

 

Mbunge Zungu wa Ilala Anaswa Akitoa Rushwa

NewsImages/6661242.jpg
Mbunge wa Ilala, Musa Zungu
Watu watano akiwemo mbunge wa Ilala Musa Zungu wamekamatwa na Taasisi ya kuzuia na Kupambana na Rushwa Mkoani Dodoma wakidaiwa kutoa rushwa kwa wajumbe wa Jumuiya ya wazazi ili wawachague.
Kamanda wa Taasisi hiyo Eunice Mmari alisema Zungu alikamatwa katika Hotel ya Golden Crown majuzi kati ya saa mbili na nusu na saa tatu usiku.

Eunice alisema baa ya taasisi yake kupata taarifa hizo walianza kumfuatilia kwa karibu mgombea huyo na ndipo walipomsikia akitoa maagizo kupitia simu ya mkononi kuagizia nani apewe kiasi gani.

Alisema baada ya hatua hiyo TAKUKURU walianza kumfatilia Zungu na ndipo waligundua kuwa yupo katika gari ndogo aina ya Toyota Mark –II huku akifuatana na gari jingine aina ya Prado ambalo ndiko fedha na wapambe wake walikuwa wamepanda.

Alisema baada ya kulisimamisha gari hilo alilokuwemo Zungu ghafla Prado hilo liliweza kutoroka na kumuacha Zungu na ndipo alipokamtwa na kuhojiwa.

Alisema hata hivyo TAKUKURU waliweza kufuatilia mitandao ya simu na kisha kubaini kuwa fedha hizo zilikuwa zikigawiwa na mmoja wa wakala wake ambaye naye kwa sasa amekamtwa.

Kamanda huyo aliwataja wengine waliokamatwa na Zungu ni pamoja na Yahya Khamis Danga , Busulo Mohamed Pazi na Famik Joseph Mang’ati.

Alisema kwa sasa watuhumiwa hao wote wameachiwa kwa dhamana huku uchunguzi zaidi ukiendelea na watafikishwa mahakamani mara baada ya kukamilika.

Aidha kamanda huyo alisema mwingine aliyekamtwa ni pamoja na Fatuma Kasenga ambaye ni mwenyekiti wa jumuiya ya Wazazi kutoka Mkoa wa Mbeya.

Alisema mwenyekiti huyo alikamatwa usiku wa kuamkia juzi, saa tisa usiku katika hoteli ya Kitoli mjini hapa akiwanunulia wajumbe wake chakula.

Kamanda huyo apia alisema kuna taarifa zaidi ambazo zinamtaja Alhaji Abdalah Bulembo kuwa naye amekuwa akitajwa sana katika utoaji huo wa rushwa.

Alisema hata hivyo wanaendelea na uchunguzi dhidi ya tuhuma za Bulembo na wamepata taarifa za awali kuwa anatoa rushwa hizo nyumbani.

Tuesday, September 25, 2012

HAKIMU WA ILALA ASOMEWA MASHTAKA YA RUSHWA KISUTU.

Hakimu na Rushwa                                                                    

 

 

 

 

 

 

 

 

 

 

 

 

 

 

 Hakimu Mkazi wa Mahakama ya Wilaya ya Ilala Pamela Kalala (kushoto),akitoka katika mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu jijini Dar es Salaam jana,baada ya kusomewa shitaka la kuomba rushwa ya Shilingi milioni tatu.Picha na Michael Matemanga

Sunday, September 9, 2012

WAZIRI MKUU MSTAAFU AMEITAKA AFRIKA IPAMBANE NA RUSHWA, AMERIDHISHWA NA UTENDAJI KAZI WA TAKUKURU.

Sumaye ameitaka Afrika kutokomeza rushwa

 
Waziri Mkuu Mstaafu, Frederick Sumaye amezitaka nchi za Afrika ikiwemo Tanzania kupambana na makundi na kuwalipua wala rushwa na wapokeaji kwa kuwachukulia hatua.
Alitoa kauli hiyo jana jijini Dar es Salaam katika maadhimisho ya miaka 20 ya Chuo Kikuu Huria cha Tanzania, (OUT).
Katika mada yake iliyokuwa ikizungumzia kuhusu changamoto za kupunguza umaskini nchini, Sumaye alisema nchi za Afrika zipo nyuma kimaendeleo na kwamba yapo mambo mengi yanayotakiwa kufanyika.
Alitaja baadhi ya mambo hayo kuwa ni nchi kuwa na serikali inayopambana na makundi yote mabaya hasa rushwa.
"Lazima tuipige vita rushwa ili kile kidogo kinachotakiwa kipatikane basi kipatikane kwa ajili ya huduma za wananchi na sio kupotea njia," alisema.
Alitaka nchi zifanye biashara ambazo zitaweza kuzimudu na kutolea mfano Tanzania.
"Tusiuze tu vitu kwa mfano magogo, pamba na madini nje ya nchi, tunatakiwa vitu hivi tuvibadilishe kuwa thamani ndio tuvipeleke nje kwenye soko la biashara, tunaiuzia magogo China halafu yeye anayabadilisha kuwa vitu vya thamani anakuja kutuuzia sisi tena, kwa nini sisi tusifanye vyote hivyo, tuwauzie wao," alisema.
Kuhusu rushwa na utawala bora, Sumaye alisema lazima nchi ifikie mahali iwe na utaratibu wa kuhakikisha jambo hilo halivumiliki kwa sababu limekuwa likiigawa jamii katika kundi la wenye utajiri na maskini.
Mtazamo wake kama Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru) kwa sasa inafanya kazi yake ipasavyo kutokana na kuanzishwa wakati akiwa madarakani, alisema anafikiri inafanya kazi yake.
Kuhusu nini kifanyike, Sumaye alisema nchi inatakiwa kuwa na utawala bora ambao utawezesha rasilimali za nchi zinatumika kwa manufaa ya watu wote.
Pia alisema nchi inatakiwa kuhakikisha inakuwa na utawala wa sheria na kuheshimu haki za binadamu na kuwepo na matumizi sahihi ya mali za taifa ili kila Mtanzania aweze kunufaika nazo.
Naye, Mkuu wa Chuo hicho, Profesa Tolly Mbwette, alisema kuwa, katika maadhimisho hayo miadhara ya majadiliano iliyotolewa imelenga jamii na serikali kwa ujumla.
Alisema lengo lake ni kutoa michango yao kwenye maeneo tofauti ambayo serikali imejiwekea katika kuyafikia maendeleo.
Profesa Joseph Mbwiriza wa OUT akichangia majadiliano hayo, alisema suala la umaskini ni kubwa na watu wengi wapo nje ya mfumo rasmi wa uchumi.
"Wanawake wengi hatuwatambui, kazi wanazozifanya haziingii kwenye takwimu zetu za kiuchumi za taifa, nini kifanyike tutekeleze Mpango wa Kurasimisha Rasilimali na Biashara za Wanyonge Tanzania (Mkurabita) ili kazi zao na za wengine zitambuliwe kisheria, " alisema.
Katika maadhimisho hayo mijadala mbalimbali ilitolewa ukiwemo uliokuwa ukiangalia kupotea kwa maadili kwenye jamii ya Tanzania.
CHANZO: NIPASHE JUMAPILI