Showing posts with label RUSHWA. Show all posts
Showing posts with label RUSHWA. Show all posts

Sunday, November 4, 2012

MBUNGE ZUNGU WA ILALA AKAMATWA KWA RUSHWA

 

Mbunge Zungu wa Ilala Anaswa Akitoa Rushwa

NewsImages/6661242.jpg
Mbunge wa Ilala, Musa Zungu
Watu watano akiwemo mbunge wa Ilala Musa Zungu wamekamatwa na Taasisi ya kuzuia na Kupambana na Rushwa Mkoani Dodoma wakidaiwa kutoa rushwa kwa wajumbe wa Jumuiya ya wazazi ili wawachague.
Kamanda wa Taasisi hiyo Eunice Mmari alisema Zungu alikamatwa katika Hotel ya Golden Crown majuzi kati ya saa mbili na nusu na saa tatu usiku.

Eunice alisema baa ya taasisi yake kupata taarifa hizo walianza kumfuatilia kwa karibu mgombea huyo na ndipo walipomsikia akitoa maagizo kupitia simu ya mkononi kuagizia nani apewe kiasi gani.

Alisema baada ya hatua hiyo TAKUKURU walianza kumfatilia Zungu na ndipo waligundua kuwa yupo katika gari ndogo aina ya Toyota Mark –II huku akifuatana na gari jingine aina ya Prado ambalo ndiko fedha na wapambe wake walikuwa wamepanda.

Alisema baada ya kulisimamisha gari hilo alilokuwemo Zungu ghafla Prado hilo liliweza kutoroka na kumuacha Zungu na ndipo alipokamtwa na kuhojiwa.

Alisema hata hivyo TAKUKURU waliweza kufuatilia mitandao ya simu na kisha kubaini kuwa fedha hizo zilikuwa zikigawiwa na mmoja wa wakala wake ambaye naye kwa sasa amekamtwa.

Kamanda huyo aliwataja wengine waliokamatwa na Zungu ni pamoja na Yahya Khamis Danga , Busulo Mohamed Pazi na Famik Joseph Mang’ati.

Alisema kwa sasa watuhumiwa hao wote wameachiwa kwa dhamana huku uchunguzi zaidi ukiendelea na watafikishwa mahakamani mara baada ya kukamilika.

Aidha kamanda huyo alisema mwingine aliyekamtwa ni pamoja na Fatuma Kasenga ambaye ni mwenyekiti wa jumuiya ya Wazazi kutoka Mkoa wa Mbeya.

Alisema mwenyekiti huyo alikamatwa usiku wa kuamkia juzi, saa tisa usiku katika hoteli ya Kitoli mjini hapa akiwanunulia wajumbe wake chakula.

Kamanda huyo apia alisema kuna taarifa zaidi ambazo zinamtaja Alhaji Abdalah Bulembo kuwa naye amekuwa akitajwa sana katika utoaji huo wa rushwa.

Alisema hata hivyo wanaendelea na uchunguzi dhidi ya tuhuma za Bulembo na wamepata taarifa za awali kuwa anatoa rushwa hizo nyumbani.

Tuesday, August 21, 2012

MKOMBOZI WA TANZANIA TOKA MAKUCHA YA RUSHWA NI MTANZANIA MWENYEWE.

 Nani ataikomboa Tanzania kwenye makucha ya rushwa?

Jenerali Ulimwengu.
HATA kwenye maandiko ya vitabu vitakatifu tunaambiwa kuwa, Mwenyezi Mungu baada ya uumbaji wa dunia alimweka Adamu na Hawa katika Bustani ya Edeni na kuwapa uhuru wa kula matunda yote katika  bustani ile isipokuwa matunda ya mti uliokuwepo katikati ya bustani.
Kwa wanaofuatilia maandiko ya dini wanafahamu kilichotokea. Hapa nchini kuna sheria na maneno mengi yanayowataka viongozi na raia wa kawaida kutojihusisha na vitendo vya rushwa.
Lakini ajabu ni kwamba hivi majuzi tumesikia shutuma nzito za vitendo vya rushwa zikitolewa ndani ya Bunge vikiwahusisha viongozi wa Kamati za Bunge hususan Kamati ya Nishati na Madini, Hesabu za Serikali za Mitaa na Hesabu ya Mashirika ya Umma.
Kiukweli  tunachokiona si cha ajabu, maana ni taswira ya mambo ambayo sisi kama jamii tumeyakubali, tumeyapokea na kuyafanya kuwa sehemu ya maisha yetu. Limekuwa ni jambo la kawaida mtumishi fulani kula rushwa na kujitajirisha harakaharaka na watu kumsifu kwamba eti ana akili sana!
Katika baadhi ya vitengo kama vile mahakamani, polisi, idara za ardhi au maliasili kama ambavyo iliwahi kuaninishwa na Tume ya Joseph Warioba, ulaji wa mlungula ni  tabia ambayo baada ya muda imegeuka na kuwa ‘mazoea’ na hatimaye kuwa haki.
Wanaofanya hivyo wanajiona wana haki ya kupewa rushwa, mahakamani mafaili yanafichwa na hata polisi, sehemu ambazo zilipaswa kuwa mstari wa mbele kutetea haki ya mtu.
Kila mtu pale alipo aiangalie jamii yetu na matendo yake nyakati hizi, naweza kusema kuwa tunaishi katika jamii ya watu wanaopenda rushwa, maana hata bei za bidhaa zipande kiasi gani hakuna mtu anayethubutu kusema kwa sauti kuwa tunalanguliwa!
Kwa kweli inasikitisha  zaidi kwa namna Watanzania na serikali yao wanavyoonekana kwa taswira ya rushwa. Hayati Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Kambarage Nyerere katika uhai wake na uongozi wake alikemea kwa vitendo rushwa na kwa kiasi kikubwa alifanikiwa kupunguza vitendo vya rushwa nchini.
 Kwa msimamo huo huduma za jamii kama vile elimu ilikidhi haja kwani wanafunzi walikuwa wakifundishwa na kugawiwa madaftari na hata kalamu bure, afya- watu walikuwa wakitibiwa bure na dawa zilikuwa zikipatikana, barabara- zilijengwa japokuwa kasi haikuwa kubwa, maji safi na salama yaliwafikia wananchi wengi vijijini bila mizengwe yoyote.
Sifa ya nchi ya Tanzania hakika ilikuwa nzuri machoni mwa wananchi na nje ya nchi. Ilikuwa ni vigumu kuona kiongozi wa serikali au shirika la umma akijenga hekalu ambalo halilingani na mshahara au kipato chake.
Leo hii kiongozi anaweza kusema kwenye bajeti ya serikali kuwa jengo fulani la serikali halitajengwa kwa kuwa bajeti haitoshi lakini huyohuyo akanunua magari yake mawili ya kifahari na kujenga nyumba mbili au tatu. Utajiuliza fedha amepata wapi? Jibu ni rahisi, ni rushwa tu.
Bahati mbaya baada ya uongozi wa Mwalimu, dhambi ya rushwa ikaanza taratibu kutambaa ndani ya jamii na sasa imekuwa kubwa mithili ya kansa isiyotibika. Tunashuhudia rushwa waziwazi katika chaguzi ambapo hata baadhi ya wana habari wanatajwa kujihusisha na rushwa. Hii ni mbaya sana. Wakati mwingine uhitaji hata ushahidi, maana maandishi yao na vitendo vyao vinajionesha.
Nimpongeze mwanahabari mkongwe, Jenerali Twaha  Ulimwengu ambaye amewataka wanahabari na wananchi wa Tanzania, hususan wale wanaokerwa na vitendo vya rushwa kukusanya hasira na kukemea kwa nguvu vitendo vya rushwa nchini, namuunga mkono mia kwa mia.
Alisema kuwa, kimsingi huwezi kupigana na mtu au nchi kama huna hasira, vivyohivyo inatupasa kuwa na hasira ya kutosha kupambana na adui huyu aitwaye rushwa ambaye kwa hakika amesababisha mabilioni ya shilingi za walipa kodi kupotea na kuingia katika mifuko ya watu binafsi wasio na huruma na wenzao.
Niseme bila kumung’unya maneno kwamba kama rushwa itaachiwa isambae bila kupigwa vita kwa nguvu, itamaliza taifa, tutateketea.
Jipu limepasuka, siwezi kuwa adui kwa kusema ukweli

Credits; www.globalpublisherstz.info