Sunday, July 22, 2012

HAKIMU ALIYETUHUMIWA KWA RUSHWA AACHIWA HURU HUKO MBEYA.

Habari na Ezekiel Kamanga,Mbeya.
Mahakama ya Hakimu Mfawidhi Wilaya ya Mbeya,umemwachia huru aliyekuwa Hakimu mkazi wa mahakama ya Mkoa wa Mbeya Amani Mwihomeke(30),aliyekuwa anakabiliwa na tuhuma za rushwa.

Hakimu huyo anakabiliwa na makosa mawili kinyume cha sheria kifungu cha 15 cha kanuni ya adhabu kifungu kidogo(i) cha 11/2007 ambapo alidaiwa kushawishi na kupokea rushwa ya shilingi 150,000 mnamo Mei 29 mwaka huu.

Mwendesha mashtaka wa Serikali kutoka kikosi cha kupambana na kuzuia rushwa nchini TAKUKURU,Kanda ya Mbeya Bwana Nimrod Mafwele akisaidiwa na Sarah Martin walidai Mahakamani kuwa Amani Mwihomeke alishawishi na kupokea rushwa hiyo katika Bar ya Bonanza iliyoko barabara ya Benki Kuu Jijini Mbeya.

Hakimu mfawidhi wa wilaya ya hiyo a Seif M. Kulita amesema mtuhumiwa anaachiwa huru kutokana na upande wa mashtaka kushindwa kuthibitisha tuhuma hizo hivyo mahakama kuchukua uamuzi huo wa hukumu ambayo ilichukua masaa matatu kusomwa katika mahakama hiyo.

Hakimu Mwihomeke alikuwa anatetewa wakili wa kujitegemea Mika Thadayo Mbise.

Hata hivyo Hakimu mfawidhi Kulita alitaka waeshesha mashtaka kuandaa vema mashtaka ambapo wameshindwa kuthibitisha tuhuma ambazo zingemtia mtuhumiwa hatiani.

Tuesday, July 3, 2012

MAKAMANDA WA JKT WAFIKISHWA MAHAKAMANI KWA UFISADI

ASKARI saba wa Jeshi la Kujenga Taifa (JKT) wakiwamo Luteni Kanali watatu, wamepandishwa kizimbani katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, Dar es Salaam wakikabiliwa na mashitaka ya kuhamisha na kupitisha Sh bilioni 3.8 kwa ajili ya ununuzi wa mali chakavu. Washitakiwa hao walifikishwa mahakamani hapo jana asubuhi na Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU), wakiwa kwenye gari aina ya Toyota Land Cruiser lenye namba za usajili T529 ASM lenye vioo vyeusi wakisindikizwa na gari lenye namba DFP 8763. Walisomewa mashitaka saba na mawakili kutoka Takukuru, Donasian Kessy na Ben Linkolin mbele ya Hakimu Mkazi Aloye Katema. Washitakiwa wenye cheo cha Luteni Kanali ni Mkohi Kichogo, Paul Mayavi na Felix Samillan ambaye ni Mkuu Miradi wa Suma JKT. Wengine ni Kanali Ayoub Mwakang’ata, Sajini John Laizer, Meja Peter Lushika na Meja Yohana Nyuchi. Wakili Kessy alidai kuwa, Machi 5, 2009 katika Ukumbi wa Mikutano wa Shirika la Suma JKT, washitakiwa wakiwa wajumbe wa Bodi ya Suma JKT, walijifanya wajumbe wa Bodi ya Kampuni ya Takopa inayoundwa kwa ubia kati ya Serikali ya Korea Kusini na Suma JKT. Alidai lengo la kujifanya wajumbe wa Bodi ya Takopa, lilikuwa kupitisha fedha kutoka kampuni hiyo kwenda Suma JKT kwa ajili ya ununuzi wa magari na mitambo ya ujenzi chakavu bila idhini ya Bodi ya Wakurugenzi wa kampuni hiyo. Wakili Kessy alidai kuwa washitakiwa walitumia vibaya ofisi kupitisha fedha hizo kwa ajili ya ununuzi wa magari pamoja na mitambo hiyo bila kufuata kifungu cha 58 (3) cha Sheria ya Manunuzi ya Umma. Aliendelea kudai katika mashitaka ya tatu yanayowakabili Luteni Kanali Samillan na Luteni Kanali Kichogo kuwa, Machi 16, 2009 walihamisha Sh bilioni 2.8 kupitia hundi namba 000010 kutoka akaunti ya Takopa namba 0111030331753 kwenda akaunti ya Suma JKT 01110307094 katika Benki ya Taifa ya Biashara (NBC). Ilidaiwa kuwa Aprili 3, 2009, wakijidai wajumbe wa Bodi hiyo ya Takopa walihamisha Sh milioni 489.7, Aprili 4 walihamisha Sh milioni 269.5, Mei 4, mwaka huo walihamisha Sh milioni 350 kutoka akaunti ya Takopa kwenda akaunti ya Suma JKT bila kuzingatia Kanuni ya 156 ya Sheria ya Fedha za Umma. Katika mashitaka ya saba yanayowakabili washitakiwa wote, ilidai kuwa kati ya Machi na Mei mwaka 2009 jijini Dar es Salaam, washitakiwa walipanga njama za kuhamisha fedha kutoka katika taasisi ya Takopa kwenda kwenye akaunti ya Suma JKT bila kufuata Kanuni 156 ya Sheria ya Fedha za Umma. Washitakiwa wote walikana kutenda makosa hayo na upande wa mashitaka ulidai kuwa upelelezi wa kesi hiyo umekamilika na kuwa hawana pingamizi la dhamana endapo washitakiwa watakidhi masharti yatakayotolewa na Mahakama. Hakimu Katemana aliwataka washitakiwa kuwa na wadhamini wawili wa kuaminika watakaosaini hati ya Sh milioni 25 kila mmoja. Washitakiwa walitimiza masharti na kuachiwa kwa dhamana hadi Agosti mosi, mwaka huu. Hata hivyo, baada ya washitakiwa hao kufikishwa mahakamani hapo, hawakuwekwa mahabusu kama ilivyo kawaida kwa washitakiwa wengine, walikaa kwenye gari hadi saa 7 mchana waliposomewa mashitaka yao